Thursday, October 24, 2013

SIWEMA

Hapo zama za kale palitokea na mama mmoja. Siku moja alipokuwa akitembea kuelekea kwenye shughuli zake za kila siku, akakutana na watu wakiwa wamebeba maiti wanaenda kuzika, mara akapatwa na uchungu wa kujifungua.

Mtoto alipozaliwa alimpa jina la Siwema. Siwema alikuwa mtoto mzuri sana kwani alikuwa mtoto mtii na mkarimu sana pale kijini kwao lakini Siwema alikuwa na tatizo la ulemavu wa kutoweza kasema, (ububu). 

Nyumba ya akina siwema ilikuwa imejengwa kando kando ya njia ambayo watu wengi walikuwa wakipita kuelekea mashambani mwao.

Wale watu walipokuwa wakipita hapo Siwema alikuwa akiwasaidia maji ya kunywa na chakula kila walipokuwa wakihitaji bila wazazi wake kuwepo.

Siku moja kuna mtu na mke wake na mtoto wao walitoka nyumbani kwao wakiwa wamepanga kwenda kuiba hapo nyumbani kwa akina Siwema. Lakini lengo lao lilikuwa kumuua kwanza Siwema ndipo waweze kufanikisha lengo lao.

Sasa walipofika pale wakamkuta Siwema akiwa amebaki peke yaka wazazi wake wakiwa wamekwenda shambani. Mara yule baba akatoa panga lake ili aanze kumkata Siwema lakini ghafula ule upanga ukaruka ukaenda ukamchinja mtoto wao aliyekuwa amebebwa mgongoni na mama yake.

Walipoona wamemuua mtoto wao wakalia kwa nguvu wakipiga kelele kwamba Siwema amemuua mtoto wao. Watu walifika wengi pale nyumbani kwa akina siwema na wazazi wake wakawa wamefika pale.

watu wote wakawa wanamtuhumu Siwema kuwa ameua. Wakamchukua wakampeleka kwenda kumshitaki. Alipofika kule Siwema alihukumiwa kunyongwa hadi kufa. Wazazi wake walilia sana kwani Siwema hakuweza kujitetea kwa sababu alikuwa hawezi kuongea.

Siku ilipofika ya kunyongwa kwa Siwema watu walijaa wengi sana kwenye eneo la kunyongea ili washuhudie sjinsi Siwema anavyonyongwa.

Siwema akapelekwa hadi pale kwenye eneo la kunyongea, alipofika tu pale ghafula akaanza kuongea huku akilia kwa uchungu sana.

Akaanza kusema, 
"kweli nimeamini binadamu si wema, kila siku watu walikuwa wakipita pale nyumbani na nilikuwa nikiwasaidia bila wazazi wangu kujua kila walipokuwa na shida zao.  Kweli nimemuamini yule mtu aliyekuwa akiondoka hapa duniani"

Watu wote wakashangaa inakuwaje Siwema leo kuongea, ikawabidi wakae kimya wamsikilize.

Siwema akaanza kuongea, "siku moja nilipokuwa bado sijazaliwa nilipishana na mtu ambaye yeye alikuwa amekufa hivyo alikuwa anakwenda kuzikwa, yule mtu aliniambia hivi,
" Nakuonea huruma sana wewe mwenzangu unayekwenda duniani, mimi mwenzako nimetoka huko lakini nilichogundua ni kwamba binadamu si mwema hata kidogo hata umfanyie nini"

Siwema alimaliza kuongea kwa kusema, "mtoto wao wamemuua wao wenyewe lakini leo wananisingizia mimi, nashukuru kwa yote mliyonitendea. Kwa herini!

Wote wakasikitika kwa yaliyotokea, wakawaita wale watu waliomsingizia Siwema, wakaulizwa na Siwema akasimulia jinsi ilivyokuwa adhabu ikabadilishwa kutoka kwa Siwema ikaenda kwa wale watu, mtu na mkewe.

NA HADITHI YANGU INAISHIA HAPO!!!!


No comments:

Post a Comment