Monday, August 12, 2013

HAKUNA FUNDI MWENGINE

Hadithi! hadithi!


Hapo zama za kale palitokea fundi wa kufua vyuma katika nchi fulani. Fundi huyo alikuwa maarufu saaaana pande zote nchini humo.

Akatoke kijana mmoja  akamfuata na kumuomba amfundishe kazi hiyo ya kufua vyuma. Fundi yule wala hakuwa na hiyana alimkubalia na akaanza kumfundisha mpaka akajua.

Baada ya kuona kwamba amejua vizuri kufua vyuma, akaanza dharau kwa yule mwalimu wake. Akawa anajitapa kila kona kwamba yeye ndiye fundi mzuri na hakuna fundi mwingine zaidi yake. Sasa ikafika wakati akawa ametunga wimbo kabisa wa kujisifu kwamba hakuna fundi mwengine zaidi yake.

Hakuna fundi mwengine
Hakuna fundi mwengine!

Wakati yule fundi mwanafunzi akiwa anaimba hivyo, yule fundi mwalimu akawa anajibu kwa upole sana,

Fundi mwengine nipo bwana,
Fundi mwengine nipo bwa!

Hatimaye zile sifa za yule fundi mwanafunzi zikamfikia mfalme wa nchi hiyo. Akawatuma watu waende wakamwite kuna kazi alikuwa anataka kumpa kutokana na umaarufu wake.


Yule fundi mwanafunzi akaitwa, akafika nyumbani kwa mfalme, mfalme akamwambia,
Mfalme: Nasikia wewe ni fundi mzuri sana hapa nchini na hakuna fundi mwengine kama wewe!
Fundi Mwanafunzi: Ndiyo mfalme.
Mfalme: Sasa kuna kazi nataka kukupa ila ina masharti kama utashindwa.
Fundi Mwanafunzi: Sawa Mfalme, nipo tayari.
Mfalme: Nataka umtengeneze mtu na awe na pumzi kama binadamu wa kawaida, nakupa wiki mbili kazi hiyo iwe imekamilika, tofauti na hapo utahukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Yule fundi mwanafunzi alitoka pale kwa mfalme akiwa amehuzunika sana huku akiwa na mawazo mengi juu ya kazi alopewa na Mfalme.

Sasa akawa analia kila siku na akaanza kudhohofika na hata zile nyimbo zake alizokuwa akiimba wakati akiwa anafanya kazi akawa haimbi tena, kwa sababu alijua kwamba hatoweza.

Yule fundi mwalimu alipomuuliza kwa nini amekuwa katika hali kama ile, yule fundi mwanafunzi alimueleza mwalimu wake yote aliyoambiwa na mfalme.

Yule mwalimu akamuonea huruma sana, akamwambia aende kwa tena kwa mfalme akamweleze kwamba ili kazi hiyo iweze kutekelezeka ni lazima kuwe na mkaa wa migomba pamoja na machozi ndoo moja.

Yule kijana akafanya kama alivyoambiwa na mwalimu wake, naye mfalme akafanya jitihada za kupata mkaa wa migomba na machozi lakini hakufanikiwa kupata.

Hivyo ile kazi ya kumtengeneza mtu ikawa imeshindikana na huo ndiyo ukawa usalama wake.

Alirudi kwa mwalimu wake akiwa na furaha na kumshukuru sana na kumuomba radhi mwalimu wake kwa yote aliyoyatenda. Kwani alikuwa amemnusuru kifo kutoka kwa mfalme.

Na hadithi yangu imeishia hapo.

FUNZO KUPITIA HADITHI HII.

Majivuno siku zote siyo kiti kizuri katika maisha yetu, hata kama kweli unaweza ukafanya vizuri zaidi ya yule aliyekupa njia ya wewe kuweza kufika hapo ulipo. Mjivuno ndiyo kitu kilichomponza shetani mpaka akatupwa motoni.

Siku zote tunatakiwa kuwa na heshima kwa wale waliotufanya tuweza kujitambua katika maisha yetu. Hata wahenga waliposema kwamba 'SIKIO HALIZIDI KICHWA' hawakukosea.

No comments:

Post a Comment