Thursday, August 29, 2013

HADITHI YA FARAJA ALIYEKATA TAMAA




Hapo zama za kale palitoka kijana mmoja aliyekuwa akijulikana kwa jina la Faraja.

Faraja alikuwa kijana mwenye bidii sana ya kufanya kazi hapo kijijini kwao hasa katika kazi yake ya kilimo. Alikuwa anahakikisha nyumbani kwake hakukosekani chakula.
Mwaka mmoja ilitokea hali ya ukame sana katika nchi yao, mazao mengi sana yalikauka na hata wanyama nao walikufa kwa kukosa chakula na maji kwa sababu ya ukame.

Faraja alikuwa amelima migomba mingi sana ya ndizi. Hivyo ndizi ndiyo kilikuwa chakula chake alichokuwa akikitegemea wakati ule wa njaa.
Akawa kila siku anakula ndizi moja, hatimaye zile ndizi zikawa zinaisha hivyo akawa anahuzunika sana moyoni atafanya nini ili kujiokoa katika janga hilo la njaa.

Akala ndizo zote, siku alipokuwa anamalizia ndizi ya mwisho akawa anawaza moyoni mwake, “nitapanda kwenye mti mreeeeefu sana na hii ndizi, nikimaliza kuila nitajirusha chini ili nife”. 

Aliamua kupanda na ndizi yake hadi juu ya mti, akala ile ndizi, alivyomaliza akatupa ganda chini.
Akawa anajiandaa kujirusha lakini alipokuwa anataka kujirusha mara akamuona bibi kizee anaokota lile ganda na kuanza kulila.

Faraja aliumia sana moyoni mwake, akaomba msamaha kwa Mungu kwa kuwa alichokuwa amepanga kukifanya hakikuwa sahihi.
“Kumbe kuna watu wana shida zaidi yangu, afadhali mimi nimkula ndizi lakini mwenzangu amekula ganda la ndizi ambalo nimelitupa!” alihuzunika Faraja.
Akaamua kuteremka toka kwenye ule mti na kurejea kwenda nyumbani kwake.

FUNZO

Katika maisha yetu tunapaswa kushukuru kwa kila kilicho kidogo tunachokipata. Kwani wakati wewe umepata hicho kidogo kumbuka kwamba kuna mwenzako ambaye amekosa kabisa.
Pia hatupaswi kukata tamaa kwa sababu tumekosa ambacho tunachokitarajia katika maisha yetu. 

No comments:

Post a Comment