Thursday, October 24, 2013

SIWEMA

Hapo zama za kale palitokea na mama mmoja. Siku moja alipokuwa akitembea kuelekea kwenye shughuli zake za kila siku, akakutana na watu wakiwa wamebeba maiti wanaenda kuzika, mara akapatwa na uchungu wa kujifungua.

Mtoto alipozaliwa alimpa jina la Siwema. Siwema alikuwa mtoto mzuri sana kwani alikuwa mtoto mtii na mkarimu sana pale kijini kwao lakini Siwema alikuwa na tatizo la ulemavu wa kutoweza kasema, (ububu). 

Nyumba ya akina siwema ilikuwa imejengwa kando kando ya njia ambayo watu wengi walikuwa wakipita kuelekea mashambani mwao.

Wale watu walipokuwa wakipita hapo Siwema alikuwa akiwasaidia maji ya kunywa na chakula kila walipokuwa wakihitaji bila wazazi wake kuwepo.

Siku moja kuna mtu na mke wake na mtoto wao walitoka nyumbani kwao wakiwa wamepanga kwenda kuiba hapo nyumbani kwa akina Siwema. Lakini lengo lao lilikuwa kumuua kwanza Siwema ndipo waweze kufanikisha lengo lao.

Sasa walipofika pale wakamkuta Siwema akiwa amebaki peke yaka wazazi wake wakiwa wamekwenda shambani. Mara yule baba akatoa panga lake ili aanze kumkata Siwema lakini ghafula ule upanga ukaruka ukaenda ukamchinja mtoto wao aliyekuwa amebebwa mgongoni na mama yake.

Walipoona wamemuua mtoto wao wakalia kwa nguvu wakipiga kelele kwamba Siwema amemuua mtoto wao. Watu walifika wengi pale nyumbani kwa akina siwema na wazazi wake wakawa wamefika pale.

watu wote wakawa wanamtuhumu Siwema kuwa ameua. Wakamchukua wakampeleka kwenda kumshitaki. Alipofika kule Siwema alihukumiwa kunyongwa hadi kufa. Wazazi wake walilia sana kwani Siwema hakuweza kujitetea kwa sababu alikuwa hawezi kuongea.

Siku ilipofika ya kunyongwa kwa Siwema watu walijaa wengi sana kwenye eneo la kunyongea ili washuhudie sjinsi Siwema anavyonyongwa.

Siwema akapelekwa hadi pale kwenye eneo la kunyongea, alipofika tu pale ghafula akaanza kuongea huku akilia kwa uchungu sana.

Akaanza kusema, 
"kweli nimeamini binadamu si wema, kila siku watu walikuwa wakipita pale nyumbani na nilikuwa nikiwasaidia bila wazazi wangu kujua kila walipokuwa na shida zao.  Kweli nimemuamini yule mtu aliyekuwa akiondoka hapa duniani"

Watu wote wakashangaa inakuwaje Siwema leo kuongea, ikawabidi wakae kimya wamsikilize.

Siwema akaanza kuongea, "siku moja nilipokuwa bado sijazaliwa nilipishana na mtu ambaye yeye alikuwa amekufa hivyo alikuwa anakwenda kuzikwa, yule mtu aliniambia hivi,
" Nakuonea huruma sana wewe mwenzangu unayekwenda duniani, mimi mwenzako nimetoka huko lakini nilichogundua ni kwamba binadamu si mwema hata kidogo hata umfanyie nini"

Siwema alimaliza kuongea kwa kusema, "mtoto wao wamemuua wao wenyewe lakini leo wananisingizia mimi, nashukuru kwa yote mliyonitendea. Kwa herini!

Wote wakasikitika kwa yaliyotokea, wakawaita wale watu waliomsingizia Siwema, wakaulizwa na Siwema akasimulia jinsi ilivyokuwa adhabu ikabadilishwa kutoka kwa Siwema ikaenda kwa wale watu, mtu na mkewe.

NA HADITHI YANGU INAISHIA HAPO!!!!


Wednesday, September 18, 2013

MWANAMKE NA PETE


Palitokea mama mmoja alikuw tajiri sana.
Alikuwa ni mfanyabiashara mkubwa na alikuwa akimiliki meli nyingi ambazo zilikuwa zikifuata bidhaa nje ya nchi na kuzileteta ndani.

Siku moja huyo mama aliwatuma wafanyakazi wake waende wakafate vyakula kwa ajili ya biashara kwani kulikuwa na uhaba sana wa chakula katika nchi hiyo.

Wafanyakazi walienda na waliporudi na vyakula yule mama akaviangalia na kuanza kulalamika kwamba hakuridhika na chakula kilicholetwa hivyo aliamuru wale wafanyakazi wakimwage kile chakula chote baharini ili wakafate vingine.

Wale wafanyakazi wakamshauri yule mama kwamba isingekuwa vizuri chakula hicho kumwaga kwani kama hakihitaji ni vema angewapa watu ambao wanashida ya chakula.

Lakini yule mama hakukubari ushauri ule cha zaidi alicheka kwa dharau na kuanza kejeli.
Alitoka nje ya meli akasimama juu kabisa kisha akatoa pete yake ya dhahabu aliyokuwa amevaa kidoleni mwake na kuanza kusema huku akiwa ameining’iniza ile pete kwenye vidole.

“Nimesema hicho chakula chote kimwagwe baharini kamwe siwezi kuwa maskini kwa kukimwaga hiki chakula, kama nitakuwa masikini basi hii pete itarudi tena kwenye kidole changu”, akachukua ile pete akaiachia baharini.

Wale wafanyakazi wakafanya kama walivyoamuriwa na bosi wao. Wakakimwaga kile chakula wakaenda kufata tena kingine.

Siku moja akamtuma mfanyakazi wake akamnunulie samaki mbichi kwani ana hamu ya kula samaki atakayempika yeye mwenyewe.

Hivyo alitaka akanunuliwe samaki asiyepasuliwa kwani alikuwa anataku kumtengeneza yeye mwenyewe.

Na kweli aliletewa samaki kama alivyoagiza. Akamchukua yule samaki akaanza kumpasua, alishtuka sana alipoona ile pete yake aloitupa kwenye bahari tumboni mwa yule samaki.

Toka siku ile yule mama akawa masikini wa kutupa, kwani mali zote alizokuwa nazo zilitoweka.

UJUMBE
Siku zote  tunaamini kwamba mtoaji kwa kila mtu ni Mungu. Hivyo kupata kwako wewe leo haimaanishi kwamba hao waliokosa ni kwa sababu ya uzembe wao.

Kwani kuna wanaopambana na kutafuta sana tena inawezekana wakawa wanatafuta na kuhangaika kuliko hata wewe ambaye unajiona kwamba umepata.


Hivyo si vema kutoa kejeli kwa wasiokuwa navyo na kama unaona unastahili kusaidia, saidia siyo unaweka NADHIRI.

Thursday, August 29, 2013

HADITHI YA FARAJA ALIYEKATA TAMAA




Hapo zama za kale palitoka kijana mmoja aliyekuwa akijulikana kwa jina la Faraja.

Faraja alikuwa kijana mwenye bidii sana ya kufanya kazi hapo kijijini kwao hasa katika kazi yake ya kilimo. Alikuwa anahakikisha nyumbani kwake hakukosekani chakula.
Mwaka mmoja ilitokea hali ya ukame sana katika nchi yao, mazao mengi sana yalikauka na hata wanyama nao walikufa kwa kukosa chakula na maji kwa sababu ya ukame.

Faraja alikuwa amelima migomba mingi sana ya ndizi. Hivyo ndizi ndiyo kilikuwa chakula chake alichokuwa akikitegemea wakati ule wa njaa.
Akawa kila siku anakula ndizi moja, hatimaye zile ndizi zikawa zinaisha hivyo akawa anahuzunika sana moyoni atafanya nini ili kujiokoa katika janga hilo la njaa.

Akala ndizo zote, siku alipokuwa anamalizia ndizi ya mwisho akawa anawaza moyoni mwake, “nitapanda kwenye mti mreeeeefu sana na hii ndizi, nikimaliza kuila nitajirusha chini ili nife”. 

Aliamua kupanda na ndizi yake hadi juu ya mti, akala ile ndizi, alivyomaliza akatupa ganda chini.
Akawa anajiandaa kujirusha lakini alipokuwa anataka kujirusha mara akamuona bibi kizee anaokota lile ganda na kuanza kulila.

Faraja aliumia sana moyoni mwake, akaomba msamaha kwa Mungu kwa kuwa alichokuwa amepanga kukifanya hakikuwa sahihi.
“Kumbe kuna watu wana shida zaidi yangu, afadhali mimi nimkula ndizi lakini mwenzangu amekula ganda la ndizi ambalo nimelitupa!” alihuzunika Faraja.
Akaamua kuteremka toka kwenye ule mti na kurejea kwenda nyumbani kwake.

FUNZO

Katika maisha yetu tunapaswa kushukuru kwa kila kilicho kidogo tunachokipata. Kwani wakati wewe umepata hicho kidogo kumbuka kwamba kuna mwenzako ambaye amekosa kabisa.
Pia hatupaswi kukata tamaa kwa sababu tumekosa ambacho tunachokitarajia katika maisha yetu. 

Monday, August 12, 2013

HAKUNA FUNDI MWENGINE

Hadithi! hadithi!


Hapo zama za kale palitokea fundi wa kufua vyuma katika nchi fulani. Fundi huyo alikuwa maarufu saaaana pande zote nchini humo.

Akatoke kijana mmoja  akamfuata na kumuomba amfundishe kazi hiyo ya kufua vyuma. Fundi yule wala hakuwa na hiyana alimkubalia na akaanza kumfundisha mpaka akajua.

Baada ya kuona kwamba amejua vizuri kufua vyuma, akaanza dharau kwa yule mwalimu wake. Akawa anajitapa kila kona kwamba yeye ndiye fundi mzuri na hakuna fundi mwingine zaidi yake. Sasa ikafika wakati akawa ametunga wimbo kabisa wa kujisifu kwamba hakuna fundi mwengine zaidi yake.

Hakuna fundi mwengine
Hakuna fundi mwengine!

Wakati yule fundi mwanafunzi akiwa anaimba hivyo, yule fundi mwalimu akawa anajibu kwa upole sana,

Fundi mwengine nipo bwana,
Fundi mwengine nipo bwa!

Hatimaye zile sifa za yule fundi mwanafunzi zikamfikia mfalme wa nchi hiyo. Akawatuma watu waende wakamwite kuna kazi alikuwa anataka kumpa kutokana na umaarufu wake.


Yule fundi mwanafunzi akaitwa, akafika nyumbani kwa mfalme, mfalme akamwambia,
Mfalme: Nasikia wewe ni fundi mzuri sana hapa nchini na hakuna fundi mwengine kama wewe!
Fundi Mwanafunzi: Ndiyo mfalme.
Mfalme: Sasa kuna kazi nataka kukupa ila ina masharti kama utashindwa.
Fundi Mwanafunzi: Sawa Mfalme, nipo tayari.
Mfalme: Nataka umtengeneze mtu na awe na pumzi kama binadamu wa kawaida, nakupa wiki mbili kazi hiyo iwe imekamilika, tofauti na hapo utahukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Yule fundi mwanafunzi alitoka pale kwa mfalme akiwa amehuzunika sana huku akiwa na mawazo mengi juu ya kazi alopewa na Mfalme.

Sasa akawa analia kila siku na akaanza kudhohofika na hata zile nyimbo zake alizokuwa akiimba wakati akiwa anafanya kazi akawa haimbi tena, kwa sababu alijua kwamba hatoweza.

Yule fundi mwalimu alipomuuliza kwa nini amekuwa katika hali kama ile, yule fundi mwanafunzi alimueleza mwalimu wake yote aliyoambiwa na mfalme.

Yule mwalimu akamuonea huruma sana, akamwambia aende kwa tena kwa mfalme akamweleze kwamba ili kazi hiyo iweze kutekelezeka ni lazima kuwe na mkaa wa migomba pamoja na machozi ndoo moja.

Yule kijana akafanya kama alivyoambiwa na mwalimu wake, naye mfalme akafanya jitihada za kupata mkaa wa migomba na machozi lakini hakufanikiwa kupata.

Hivyo ile kazi ya kumtengeneza mtu ikawa imeshindikana na huo ndiyo ukawa usalama wake.

Alirudi kwa mwalimu wake akiwa na furaha na kumshukuru sana na kumuomba radhi mwalimu wake kwa yote aliyoyatenda. Kwani alikuwa amemnusuru kifo kutoka kwa mfalme.

Na hadithi yangu imeishia hapo.

FUNZO KUPITIA HADITHI HII.

Majivuno siku zote siyo kiti kizuri katika maisha yetu, hata kama kweli unaweza ukafanya vizuri zaidi ya yule aliyekupa njia ya wewe kuweza kufika hapo ulipo. Mjivuno ndiyo kitu kilichomponza shetani mpaka akatupwa motoni.

Siku zote tunatakiwa kuwa na heshima kwa wale waliotufanya tuweza kujitambua katika maisha yetu. Hata wahenga waliposema kwamba 'SIKIO HALIZIDI KICHWA' hawakukosea.

Thursday, June 27, 2013

NAMPENDA BIBI


Ni mara kadhaa nimewahi kusikia maneno yakitoka kwenye vinywa vya watu wakisema vibaya juu ya malezi ya akina bibi. Wengi wamekuwa wakiwakataza hata watoto wao kwenda kwa bibi zao kwa madai kuwa, akina bibi wanalea kijukuu hivyo wanawaharibu watoto kwa watawadekeza.

Bibi kwangu naweza kusema ni zaidi ya MLEZI. Nayasema hayo kwa kuwa mimi mwenyewe ni shahidi wa hilo kwa kuwa nimeishi na bibi toka nikiwa na umri wa chini ya miaka mitano hadi kufikia umri wa ujana nilionao.

Kikubwa kwake nilichojifunza ni UPENDO! Siku zote bibi hataki kuona au kusikia mjukuu wake akipata shida siyo kwa sababu anamdekeza mjukuu hapana, ila kwa sababu anampenda mtoto wake hivyo hapendi kuona mwanaye akipatwa na matatizo katika malezi. (wote tunajua ugumu wa malezi kwa watoto ulivyokuwa mgumu).
Na kwa sababu ya upendo huo ndiyo maana anaonekana kwamba hajui kulea, lakini tujue kwamba tunakosea tunapoyasema hayo. Kama wewe umelelewa na huyo huyo mama je inakuwaje akawa mlezi mbaya kwa mwanao!
Na siku zote tunatakiwa kujua kwamba akina bibi hushiriki maumivu ya mtoto wake endapo mtoto wa mtoto wake atapatwa na matatizo.

Bibi mara nyingi alitumia hadithi katika kufundisha mema na mabaya, kweli ni vigumu au ni mara chache sana kumuona bibi akishika fimbo kumchapa mjukuu. Kama akigundua wewe ni mvivu, mbeya, mchoyo, mwizi, una wivu bibi atatumia hekima zake ili kufikisha ujumbe kwako juu ya madhara ya mambo hayo. Mengi niliyokuwa nikiambiwa na bibi nimeyaona kama siyo kwangu mwenyewe kunitokea basi kupitia kwa wenzangu.

Bibi ni mlezi mzuri sana tena sana, kamwe hawezi kushindwa kumlea mwanao. Kama atashishindwa basi hata kwako atakuwa alishindwa.
Hivi karibuni nitawashirikisha wale ambao walikosa nafasi hiyo ya kukaa na bibi kwa mawazo ya wazazi wao kwamba bibi zao wangewaharibu, yale ambayo mimi nimeyapata kwa bibi. kupitia hadithi!!!


NAKUPENDA SANA BIBI, HESHIMA KWA AKINA BIBI WOTE DUNIANI!!!